Ijumaa, 11 Septemba 2015

NGUVU NA MUDA VIKIISHA MWENYE MAONO ATAFANYA NINI?

NGUVU NA MUDA VIKIISHA MWENYE NDOTO ATAFANYA NINI?

WHAT WOULD A DREAMER DO WHEN THEIR ENERGY IS GONE OR THEIR TIME IS OVER?

Hapa Sinza kuna mahali panaitwa Sinza Makaburini. (Nadhani unaelewa kwa nini panaitwa hivyo). Kuna siku nilikuwa narejea nyumbani kutoka kwenye "mishe mishe" zangu. Late night. Saa nne hivi usiku. Nikapita eneo hilo upande zinakopaki taxi kwa wanaopafahamu. Niko natembea kwa mguu. Nimechoka. Ninawaza mambo yangu yalivyoenda siku hiyo. Ghafla nikasikia sauti ndani mwangu from nowhere inanambia: "Angalia hilo kaburi palee". Of course nikaangalia. Ile sauti ikaniambia hivi: " Huyo mtu alikuwa na ndoto kubwa kuliko za kwako, lakini nilishamchukua. Hayupo tena duniani" Halafu basi sauti ikapotea. Can you imagine? Kwanza moyo ukadunda balaa.. Si unajua..? Teh. Halafu akili ndo ikarejea japo hayo yote yalikuwa kama ndani ya sekunde 10 tu hivi!! Nikajua Mungu alikuwa anasema na mimi kitu kuhusu ndoto zangu. Maana yake yule mtu kwenye lile kaburi MUDA wake uliisha kabla ndoto zake kubwa (kuliko za kwangu) kutimia. Na ndivyo inavyokuwa kwa watu wengi. Nilifikiria usiku wote siku ile. Ni true story hii. Niliwaza sana kuhusu maisha yangu that night.

Hii inanirudisha miaka kadhaa iliyopita. Nilipokuwa nimeajiriwa.  Nilipenda sana kuwahi kazini alfajiri ili kupata muda wa kuomba, kusoma vitabu na kuota ndoto zangu za maisha.  Stanbic Bank HQs...Sehemu ambayo sitaisahau kwa sababu ya mambo meengi sana ikiwemo jambo hili. I will always love that place. Mara nyingi nilifika kazini saa 12 kasoro na hivyo nilikuwa na muda mwingi wa kukaa parking kusoma kuomba na kuota ndoto zangu mpaka saa moja na nusu yaani nusu saa kabla ya muda wa kazi. Huo ulikuwa ulimwengu mwingine. Ulimwengu niliokutana na Mungu kila asubuhi halafu baada ya hapo nikawa na kina Robin Sharma (The Monk Who Sold His Ferrari, Who Will Cry When You Die, Family Wisdom, Leadership Wisdom, The Leader Who Had No Title), kina Ryuho Okawa (An Unshakable Mind), Napoleon Hill (Think and Grow Rich), kina Robert Kiyosaki (Rich Dad Poor Dad na Cash Flow Quadrant) Zig Ziglar (How to Raise Positive Kids in a Negative World) Sergio Bambaren (The Dolphin - Story of a Dreamer) na vingine kadha wa kadha..

Kama umewahi kusoma kitabu ukahisi mwandishi alitumwa akuandikie wewe basi ndo ilivyokuwa kwangu. Nilipata mawazo mapya chanya na vitabu vilinipa pia nguvu na mwamko mpya wa kuota ndoto upya. Ndoto nzuri. Ndoto kubwa. Vitabu vilinifanya nione maisha yangu kwa mtazamo mpya na mpana. Ndoto zangu ziliongezeka ukubwa kila kitabu kipya kilipoingia ufahamuni mwangu. Mwishowe nikaona niache kazi (ku-resign) ili kuzifuata ndoto zangu mpya.

Halafu nikaanza safari ya kuzifuata ndoto zangu. Sasa hapa ndo nataka kuongelea zaidi leo.

Kuna mambo kadhaa niliyoyaobserve wakati naanza kuzifuata ndoto zangu.

MTAZAMO WA VIJANA
Vijana wengi wa rika langu au chini yangu walihisi nimepata dili jipya au nimepata kazi nyingine ya maana nk. Na wengine waliojua nataka kuanza maisha ya biashara hawakujali sana (kuhofia) kuhusu maisha yangu yatakuwaje maana walijua bado ni kijana na nikishindwa huko niendako labda ntarudi kazini hata kama siyo pale. Kwa kifupi mtazamo wa vijana walio wengi ulikuwa "GO GET IT MAN" au "SEE YOU MAN". Whatever it was. Walichukulia "poa" tu ngoja kijana akaangalie ustaarabu mwingine mwenyewe. Lakini wengi wao hawakuwa tayari kufanya maamuzi binafsi ya aina hiyo.

MTAZAMO WA WATU WAZIMA
Kwa heshima kubwa ya watu wazima wengi nilijifunza kitu kikubwa sana kwao katika kipindi hiki. Asilimia 99% ya watu wazima wote niliokutana nao kipindi hicho walinishauri nirudi kazini kwanza, na wengine walinioffer ajira kwa kuona potential waliyoifahamu ndani yangu, na wengine kunihofia sana kuhusu future yangu ingekuwaje bila ajira ya kueleweka iikizingatiwa kuwa niliacha kazi katika ofisi yenye jina kubwa mjini ambapo vijana wengi wangependa kufanya kazi. Tena ajira ya kwanza maishani halafu baada ya miaka miwili tu ya kuajiriwa.
Kitu walichofanya wote hawa ilikuwa kunishauri kama watu wanaonijali kabisa na nitawashukuru kila siku kwa kunijali hivyo. Lakini sikufuata ushauri wao licha ya kuwaheshimu sana. Sikufuata ushauri wao  sababu tu ya nguvu ya ndoto na maono yangu ambayo wengine sikuwa na uwezo wa kuwafafanulia katika lugha ambayo wangeielewa. Kiukweli wapo walioniona "much know" na wengine waliodhani "nimetupiwa" kitu. Wengine waliona nina haraka na maisha. Na kiukweli wote niliwaelewa tu.
Lakini niliona jambo fulani pia kwa kundi hili la watu wazima. Tulikuwa tukitazama suala la ku-RISK kwa macho tofauti kabisa. Au lensi tofauti. Lensi mbinuko na lensi mbonyeo.
Kilikuwa kipindi muhimu sana kwangu.

MTAZAMO WANGU BINAFSI
Kitu kikubwa nilichokiangalia zaidi ya vyote ni mtazamo wangu binafsi. Nilikuwa nikiwaza zaidi kuhusu uhusiano wa NDOTO ZANGU na NGUVU ZANGU. Nilijua nguvu zangu zilikuwa zikiongezeka kama kijana zinaongezeka lakini sikujua lini zitaanza kupungua. Na hilo lilinifikirisha sana. Nilizingatia sana hilo na kuona ni vema nianze kutumikia ndoto zangu ningali na nguvu zangu mifupani mwangu.....

~ Nianzishe vitu na kushindwa ningali kijana ili nijue mapema nini hakifanyi kazi.
~ Nianguke mara nyingi na kuinuka mara nyingi zaidi ningali na nguvu za kunyanyuka mara nyingi zaidi.
~ Nijue mimi ni mtu wa aina gani mapema na kurekebisha yanayonipasa kurekebisha kila inipasapo..ningali kijana.
~ Nisafiri huko na kule kujenga msingi wa kutimiza ndoto zangu ningali na nguvu na muda wa kufanya hivyo...ningali kijana.
~ Nithubutu kujaribu mambo magumu mapema ningali na nguvu za kupambana.. Ningali kijana.
~ Nichekwe na kusemwa mapema ningali na moyo wa kutosononeka nikichekwa.. ningali kijana.
~ Niutest uwezo wangu wa kufikiri na kuijaribu akili yangu pasipo vyeti vya shule wala CV
~ Niwaandikie watoto na wajukuu Mungu atakaoikirimia familia yangu historia ya wao kuiga na kujifunza mapema. Ningali kijana.
~ Nijifunze namna ya kuandaa watu wa kwenda nao kwenye kutimiza ndoto na maono yangu na watu wa kuyaendeleza nitakayoanzisha..ningali kijana.
~ Nijifunze wapi pa kupata msaada nitakapokuwa peke yangu bila mtu yeyote wa kunisaidia bila godfather, bila mjomba, bila pesa benki, bila mali, bila cheo, bila kutumia jina kubwa la kampuni, bila cheti chochote.

NILICHOJIFUNZA SO FAR..
Pamoja na kwamba ndo kwanza safari yangu imeanza lakini ninamshukuru Mungu kwa maamuzi niliyoyafanya. Ni karibu miaka mitano sasa na nimejifunza mambo mengi na ya msingi sana sana katika kipindi hicho kifupi. Najua safari ya kutimiza ndoto zangu ndo imeanza. Yaani nikiangalia ndoto zangu na nilipo sasa hivi ndo kwanza "majogoo". Ndo nafungasha mabegi kuanza safari. Ila sasa ramani ninayo. Siyo kama nilipoanza miaka minne iliyopita. Namshukuru Mungu kuna mambo muhimu ya msingi kuhusu hiyo safari nimeshayapata. Nimefanya makosa mengi sana, sana, na siwezi kusema sasa nimeshamaliza kufanya makosa. La hasha. Makosa mpaka kina Jack Ma, Richard Branson, waliobobea kwenye ujasiriamali bado wanafanya makosa mpaka leo. Ila ninamaanisha tu makosa ya mtu anayeanza biashara mengi nimeshajifunza. Lengo langu ni kukutia moyo kuanza kufuata ndoto zako mapema. Maana kuna kukosea kwingi na inahitaji muda wa kuweza kujifunza kutokana na makosa.. Kuna kupotea kwingi pia na kurudi tena pale ulipopotelea kuanza moja. Kama ukipotea ukiwa na miaka 60 unaweza kusema dah basi tena. Lakini ukipotea  ukiwa na miaka 25 je, si ni rahisi kurejea na kuanza moja tena maana umri na nguvu vinaruhusu. Ukiwa na miaka 60 ukigombea Ubunge unataka upate tu iwe isiwe maana miaka imeenda. Ukiwa na miaka 24 je? Kupata au kukosa inakuwa kama siyo ishu kivile. Ndo nachomaanisha hapa.

Watu wengi huwa na ndoto kubwa. Kuliko za kwangu. Kama yule mtu kwenye kaburi. (Usisahau)
Lakini hawana uthubutu wa kuzifuata ndoto hizo MAPEMA kwa gharama iwapasayo. Kwa hiyo wanabaki na frame nzuri ya vioo ukutani ambayo haina picha yoyote ndani yake. Hawajui thamani ya fremu ni picha iliyopo ndani yake.
Watu wengi wanakaa na kufurahia kichwani ndoto zao na kuona namna zitakavyokuwa nzuri SIKU ZIKITIMIA. Halafu wanafuta vumbi kwenye fremu tupu ya vioo. Ili iwe safi. Bila kujua nguvu za kutimiza maono ni nyingi zinahitajika. Na muda huenda ukawa mchache sana. Wana fremu na picha imebaki kichwani. Hawataki kujifunza kuchora picha zao wenyewe.  Wanatumia muda wao mwingi na nguvu zao nyingi kuchora picha za watu wengine. Wao wako na fremu tupu. Na picha zao zingechorwa ni nzuri mno kuliko za huyo wanayemchorea. Wanafurahia asante kutoka kwa mwenye picha inayochorwa. Wanadhani ndiyo mwisho.
Muda unakwenda nguvu zinapungua.

Halafu wanastuka muda ukiwa umeenda. Moyo wa kurisk ukiwa umeanza kupotea. Hamu ya kuchora picha zao ikiwa imeshaanza kupotea, nguvu za kukimbizana na makopo ya rangi zikiwa zimeanza kupungua au hata kwisha. Nadhani unanielewa. Utayari wa kujichafua kwa rangi na kuchekwa ukiwa umeshapotea. Reality inawakumbusha kuwa inabidi wachore picha zao mwenyewe (kutimiza ndoto/maono) kama kumbukumbu kuwa waliwahi kuwepo duniani pia. Wanakuta moyo wa kuchora haupo tena. Fremu pia zilishapata kutu. Hazina mvuto tena. Halafu picha waliyokuwa nayo kichwani wakiwa vijana wanahisi huenda waliona vibaya. Labda ulikuwa ujana. Kuota ndoto kubwa kubwa. Mbona wengine wamezeeka bila kuchora. Labda ni sawa tu kutochora. Akiwaza waliochora picha zao wenyewe anajisemea hao wana bahati sana. Anakufa na ndoto kichwani. Kama yule mtu kwenye lile kaburi.

Angalia sana jambo hili. Huenda pia una ndoto kubwa kuliko za kwangu. Angalia Mungu asije kukutolea mfano kwa wenye ndoto wengine. Kuwa ulikuwa na ndoto kubwa weeee kichwani mpaka muda wako ukaisha.

Huenda huu ni ujumbe muhimu kwako. Kama ndivyo fanyia kazi. Watu wengi huua ndoto zao wakiwa na miaka 20 hadi 30. Baada ya hapo wanaishi ndoto za wengine.
Usiwe miongoni mwao Mungu hawezi kukutolea mfano halafu asikudai. HAKIKA atakudai.
"Ulifanya nini na ndoto niliyokupa kichwani mwako?"
"Ulifanya nini na maono niliyokuwekea moyoni mwako?"
Mungu atakuuliza.
Sasa sijui utamwambia "Ulinipa (ndoto/uwezo/kipaji) kidogo nikaamua kukitunza ili nisije nikakiharibu angalau nikirudishe kwako kikiwa intact" Unajua atakujibuje? Kasome Mathayo 25:28-30 kuna mfano unaohusu hili jambo squarely.
Au utamwambia Mungu nirudishe tena tafadhali nimejifunza. Wazungu wanasema WHEN THE CURTAIN IS DOWN THE SHOW IS OVER hata kama uliipenda vipi show ikiisha imeisha. Pazia likishushwa show imeisha.
Kama yule mtu kwenye kaburi.

Kumbuka tu tena nguvu na muda wako vikiisha utafanya nini na ndoto zako kubwa kichwani? Kama nilivyouliza kwenye title ya ujumbe huu: NGUVU NA MUDA VIKIISHA MWENYE NDOTO ATAFANYA NINI?
Do something before it's curtain time for you!

Yes better do something now. And good luck. Walimu wa kukufundisha wapo wengi tu.
Wewe tu.

Na kama unatamani kujifunza chochote kwangu binafsi nitafute tu kwa WatsApp #o752366511.

When my curtain is down I want to be done with my race.
What about YOU?


Semper Fi,

ANDREA G. MUHOZYA
DAR ES SALAAM, TANZANIA,
EAST AFRICA.

WITO KWA NDUGU ZANGU WA MIKOANI

.
🚴 WITO KWA NDUGU ZANGU WA MIKOANI 📚📖

Ni siku #nyingine tena. Na leo niongee kitu kingine tena. Huenda umeshasoma message zangu nyingi hasa LIFE BEGINS AT 40  (uhalisia wa maisha huanza ukifika umri wa miaka 40) ya kwanza na ya pili ambazo zimesomwa na watu weengi zaidi toka nianze kuandika. Usisome tu ukaishia kuwaforwadia wengine  halafu ukaachia hapo. Fanyia kazi.

Okay.. Nimekuwa nikisafiri nchi hii huku na kule kwa shughuli binafsi na pia biashara. Okay safari za ndani ya nchi zinakufanya ujue nchi yetu hii ikoje kama vile safari za nje zinavyofanya ujue nchi zingine maisha yakoje.

Safari nyingi huwa nasafiri kwa njia ya mabasi. Nimekuwa nikijifunza mengi sana kutoka kwa watanzania wasafiri wenzangu. Na mojawapo ya vitu nilivyojifunza ni kuwa UKITAKA KUJUA MTU ANAWAZA NINI ANGALIA VITU ANAVYONUNUA.

Ukiwa stendi ya Ubungo kuna wachuuzi  wa vitu mbalimbali mle ndani wanapita yalipopaki mabasi madirishani na wengine huingia ndani ya mabasi. Wengi wanauza maji, mikate, juisi, matunda, magazeti, vitabu, leso, simu, flash, power bank, miwani, nk. Sasa ukiwa pale unaweza kuona mtu ananunua kila kitu kwenda nacho huko mkoani lakini siyo KITABU.

Sasa huwa najiuliza. Hivi nyie ndugu zetu kutoka huko kwetu mikoani mkija Dar huwa mnaona tu nguo na juisi na mikate vitabu hamuoniiiiii au????? Mtasema labda vya kidhungu.. Mbona vya kiswahili vipo viiingi tu..!!
Mbinu za Kupata Kazi
Mbinu za Kufanikiwa katika Maisha
Mbinu za Kufanikiwa Katika Biashara.
Mbinu za Kuanzisha Biashara.
Siri za Kutoka Umaskini Hadi Mafanikio
Mbinu za Kupata Mtaji
Mbinu za Kupata Masoko..
Nk nk

Hivi hamjaona tu..? Yaani kila siku mnanunua tu magazeti kuona nini kipya leo toka enzi na enziiii na enzi.. Vichwa vya habari vya magazeti havitabadili maisha yako. Ulishasoma habari ngapi:

MKAPA ANG'AKA..
KIGOGO TANESCO AFUMANIWA..
MWINYI APIGWA KIBAO..
ULIMBOKA SIRI NZITO..
DR BILALI AIBUKA..
JK NJE TENA..
BUNGENI HAPATOSHI..
TAIFA STARS HOI..
KIKWETE ABADILI MAWAZIRI..
MADAKTARI WASALIMU AMRI..
PINDA AMWAGA MACHOZI BUNGENI..
MANGU IGP MPYA..
GWAJIMA HALI MBAYA..
LOWASSA TISHIO CCM..
SELELI AHAMIA CHADEMA..
nk nk!

Nunueni vitabu aisee. Mna uwezo wa kuibadili nchi hii na kubadilisha taswira ya maisha huko bila kuhitaji watoto waje wajenge huko. Mtajenga wenyewe na hawa wanaokatalia mjini mtaona wanakuja  tu. Vitabu vina maarifa mengi sana na huenda ukawa hujajua hilo bado.
~ Vitabu ni vitamu kuliko juisi ya Azam.
~ Vitabu vinakata kiu kuliko maji ya Uhai
~ Vitabu vinatoa habari muhimu sana kuliko ITV
~ Vitabu vinaleta matokeo mazuri sana kuliko Simba 5 Yanga 0
~ Vitabu vinajenga msingi imara zaidi kuliko Twiga Cement
~ Vitabu vitakufikisha mbali zaidi ya basi la Shabiby

Sijui niseme nini zaidi ili twende sawa?
Utajiri mkubwa uko huko mikoani lakini sababu ya kukosa maarifa utajiri huo utafaidiwa na watu wa Kinondoni na siyo Simiyu au Njombe. Someni vitabu. Vitabu vitawafanya mpate maarifa ya kumiliki uchumi na utajiri ambao Mungu aliuweka kwenye mipaka yenu. Sasa nyie mpo mpo tu halafu mmekaa na ardhi ipo tu mnalishia ng'ombe miaka nenda rudi mpaka inamomonyoka mnahamia ardhi nyingine ugomvi kila siku na wakulima.  Ufugaji wa kisasa upo hamjui kwa sababu upo kwenye vitabu. Mna uwezo wa kumilikishwa ardhi mkaitumia kufanikiwa ila maarifa hayo hayapatikani kwenye front page ya Nipashe. Someni vitabu. Mtaishia kuchoma moto mashamba ya wawekezaji au kuvamia migodi na bado maisha yenu hayatabadilika. Mtaishia kuchagua viongozi wakawawakilishe bungeni halafu nyie mkae mnywe viroba na kusikiliza bunge redioni na kusubiri maisha bora. Ndo maana na wao wamelifanya bunge kama sehemu ya kubadilishia maisha yao. Mtabadili wabunge, mtabadili vyama, mtabadili mpaka nguo badala ya kuvaa kijani mvae nyekundu na blue lakini nasema hivi kama hamna maarifa nyinyi wenyewe mtakaa kweli kweli.

Sikia, kipato chako hakiongezwi na mwajiri wako au serikali. Ni wewe mwenyewe. Lakini kama unachonunua wewe ni vocha, juisi na magazeti aisee daah utakaa sana. Mwanamama mmoja maarufu wa Ujerumani Helen Keller ambaye alizaliwa kipofu aliwahi kusema: KITU KIBAYA ZAIDI YA KUZALIWA KIPOFU NI KUZALIWA NA MACHO YANAYOONA HALAFU UKAKOSA UWEZO WA KUONA MBELENI (SIGHT without VISION). Sasa uwezo wa kuona mbeleni unakuja kwa maarifa.
Hata Biblia inasema WATU WANGU WANAANGAMIA KWA KUKOSA MAARIFA. Unaona mambo hayo? Ukombozi wako uko mikononi mwako mwenyewe. Ukombozi wa familia yako si kazi ya bosi wako.
Mafanikio ya kizazi chako si kazi ya Serikali. Kama hutaki kukubali endelea kumsubiri Magufuli aje akufanye wewe uanze kutumia jiko la umeme au gesi badala ya mkaa. Utashangaa nyumba yako iko karibu na bomba la gesi lakini unapikia kuni. Halafu unalaumu serikali. Soma vitabu upate maarifa. Utashangaa namna utakavyopata MTAZAMO tofauti sana kuhusu maisha. Kila kitu chako kitabadilika. Hutolaumu mtu wala serikali.
Sasa nyie kujisomea bado..haya basi hata kuwasikiliza watu waliojisomea hamtaki. Au uongo? Nyie mnataka kusikikiza politiki tu. Akija #Slaa, au #Magufuli au #Zito Kabwe haooo mnajaa. Akija #EricShigongo au James Mwang'amba hata hamwendi. Sijui hata kama mnawajua.

Halafu na nyinyi wasomi mlioko mikoani hivi mmeenda kugonga mihuri tu na kusaini mafaili jamani. Hebu watu waone mkiiathiri jamii kwa kuambukiza watu hamu ya kutafuta maarifa. Sasa wewe mwalimu wa Sekondari au afisa wa serikali au meneja wa benki mtu akija kwako kumejaa CD za bongo movie na magazeti ya Udaku. Umenunua bodaboda kuna kijana anaendesha anakuletea posho jioni unaona maisha yameishia hapo. Hebu waonyesheni mfano watanzania huko mliko. Someni vitabu. Na wataanza kuiga mfano na wengi mtajikuta mnapata maarifa sahihi. Huko huko Simiyu, Namanga, Mtera, Kasulu, Dumila, Shirati, Bihalamuro, nk mtafanikiwa kweli na kuwafanya watu wakutafute wewe kujifunza mafanikio. Haijalishi elimu yako. Amua tu kuanza kusoma vitabu. Sasa nyie stendi za huko kwenu mnauza vitunguu tu na nyanya na vikapu na mahindi ya kuchemsha hakuna mwenye wazo la kuuza vitabu? Haya Sasa hata mkija huku mnataka bado mnunue mahindi na juisi na karanga halafu basi. Hebu badilisheni hilo mtaona mabadiliko makubwa sana. Kumbuka tu wapo watakaokucheka lakini ipo siku watakuita uwafundishe kuhusu mafanikio!
Tena utaitwa mpaka huko mjini. Mnaweza kufanikiwa huko huko mkajenga hoteli zenye hadhi kubwa na utalii ukafika huko mkaingiza kipato zaidi. Huko huko mkajenga Shule zenye hadhi.. Huko huko maendeleo yakawafata. Makampuni yatawafata. Watalii watawafata. Siyo kila siku watalii wanaishia Arusha tu Ruaha na sehemu kama hizo. Maarifa ni muhimu sana. Soma vitabu. Anza leo. Hakika mtakubali haya maneno siku moja.

Kama unataka kujua zaidi kuhusu vitabu vya kukusaidia, ama kuhusu wazo la biashara, ama mambo ya elimu ya mafanikio kwa ujumla WatsApp #o752366511.

Semper Fi

Andrea G Muhozya
Dar es Salaam, Tanzania
East Africa.

Nimerejea...

Kwa muda mrefu nimekuwa kimya kidogo lakini sasa nimerejea.

Mungu awabariki.

Andrea Garsper Muhozya