Alhamisi, 12 Oktoba 2017

WEWE PIA ULIFUNDISHWA KUTAFUTA THAMANI YA "X"?



Mungu ni mwema tunakutana tena. Leo naanza na swali la mathematics kutukumbusha tulikotoka! Hahaaa wale wenzangu HGL na KLF tupo?

::::::::::::::::::::::::::::::::

SWALI:

X + (1⁄2)X + 1 = 100

Tafuta thamani ya X

::::::::::::::::::::::::::::::::

Kuna makundi mawili ya watu hapa. Kuna kundi ambalo swali hilo hapo juu nyuso zitakunjamana kwa kujaribu kufikicha akili. Tutaanza kujiuliza tena nani kachanganya hiyo herufi na hizo namba tena. Kisha tutajiuliza tena sasa hii "X" naanzaje kutafuta thamani yake na kujaribu kukumbuka siku mwalimu anafundisha hivyo vitu alivaa shati gani. Na hivi MAGAZIJUTO inamaanisha nini vile?

Kifupi tutatumia muda mwingi kufikiria kuhusu swali kuliko kutafuta jibu. Na pengine tutapotezea tu.

Lakini kuna baadhi yetu nyuso zitakuwa na tabasamu hata sasa hivi walivyoona hilo swali. Wanakumbuka mbali sana. Watakumbuka walivyokuwa wanafurahi kupata mtihani wenye maswali "marahisi rahisi" kama haya. Kwenye mtihani wa hesabu hao ndo walikuwa wanaweza kukufanya ukapanic kama wamekaa pembeni yako wewe unayejiuliza kwa nini wamechanganya herufi na namba kwenye swali moja.

Na sasa hivi hapa wanaweza kuwa washakokotoa thamani ya X kwenye hilo swali na wameshaipata siku nyiingi wakati sisi wengine tulivoona tu swali tumepata allergy reactions tofauti tofauti.

Huko ndiko tulikotoka. Kwa nia njema kabisa ya watunga mitaala ya kutusaidia kufikirisha bongo zetu vizuri walihakikisha maswali kama hayo ni sehemu ya mafunzo yetu. Tulikaa muda mwingi tukifundishwa vitu vya aina hii.

Lakini sasa wote tupo kapu moja. Ndo maana sasa naomba ujiulize... Ni wapi uliwahi kufundishwa KUTAFUTA THAMANI YAKO MWENYEWE?

Yes, lini uliwahi kufundishwa kuhusu kutafuta thamani yako mwenyewe? Wewe ni nani?



Kwa wengi hilo bado.

Na kukosekana kwa fursa hiyo kumefanya watu wengi kuishi kwa kutafuta thamani ya VITU VINGINE (thamani ya X) badala ya kutafuta thamani yao wenyewe.

Tunaishi kwenye dunia ya watu ambao wanachojua ni kutafuta thamani ya X. Hawajui thamani yao wenyewe na hivyo ili kuondoa hali ya kutothaminika wanajifungamanisha na X. Kuna ambao X yao imekuwa ni magari na majumba. Ndo wanachotafuta. Wakikipata wanagundua kuna kitu bado hakiko sawa.


Kuna ambao X yao ni kujua kuongea kiingereza. Kuna ambao X ni kupata elimu ya "juu".


Wakiipata wanagundua kiukweli kwamba hiyo kumbe siyo kila kitu. Lakini wakati wanaitafuta usijaribu kuwaambia kitu kingine. Wana apply MAGAZIJUTO.

Hivi karibuni nikakutana na binti mmoja amejaribu kuapply chuo mwaka jana akakosa. Mwaka huu pia amejaribu akakosa. Akanipigia kuomba ushauri kuwa anasikitika wenzake wanapiga hatua yeye yuko tu pale pale. Nikamuuliza maswali machache na kugundua anafikiri thamani yake ipo kwenye elimu ya "juu".

Lakini uzoefu unaonyesha otherwise.
Mfano. Katika vijana wa kiume wenye thamani katika kuitangaza nchi hii yumo Mbwana Samatta na Diamond Platnumz.



Ukijumlisha elimu ya darasani ya hao wote wawili ni ndogo kuliko wengi wetu. Lakini VALUE zetu katika jamii je? Thamani ya mmoja wa hao vijana Mungu aliiweka kwenye KOO na ya mwingine Mungu aliiweka kwenye MIGUU. Kuna watu wana degree nyingi mno nchi hii lakini  thamani ya mchango wao kwa taifa HUENDA haifiki hata nusu ya ile ya Mbwana Samatta tu.

Nikamuuliza binti yule. "Unadhani Mungu alikuumba uje ufanye nini duniani?". Akasema "kwa kweli sijui kakangu". Nikamwambia basi acha kwanza kutafuta THAMANI YA X tafuta kwanza kujua thamani yako Mungu aliiweka wapi.  Akaomba nimpe wiki moja kujitafuta vizuri. Namwonbea Mungu amsaidie kujua wapi thamani yao ipo.

Kuna watu wamesoma hadi chuo kikuu lakini thamani yao imekuwa kuwa MC. Kusherehesha. Basi.
Cha ajabu kuna watu hawana degree lakini thamani yao imekuwa kwenye KUFUNDISHA. Hebu tafakari mtu kama Eric Shigongo mpaka sasa ameshafundisha vijana wangapi?


Lakini kuna watu wana Ph.Ds na kumfundisha mtu kuhusu maisha ya kawaida tu ni shida. Why? Huyu wa PhD huenda thamani yake iko kwenye USHAURI au UTAFITI. Siyo kufundisha.

So unatakiwa ujifunze kuangalia wapi Mungu aliweka TALANTA zako. Na ni ngapi alikupa. Tafuta thamani yako. Achana na kutafuta thamani ya vitu vingine ambavyo unahisi vitakupa furaha lakini mwishoni mwa maisha yako utagundua huna furaha tena na wakati vitu ulivyotafuta unavyo tayari tena vingi. Maisha halisi ni kuishi kwa kutambua thamani yako.

Kutojua thamani kumewafanya mabinti wakatoa rushwa ya ngono kwa kisingizio cha kusaidiwa ajira. Hujajua thamani yako halisi my sister. Kutojua thamani zao kumewafanya mabinti wengine kutamani kuolewa na watu wenye mali na uwezo badala ya kutafuta kuolewa na mtu aliyeumbwa kuja kuwa mume wake.

Kutojua thamani yao kumewafanya vijana wa kiume kutamani kuwa na  girlfriend au mke mwenye shepu nzuri bila kujali ni nini analeta kwenye maisha yake. Wake wengi za matajiri siyo wenye mishepu ya kutisha kama unayoona kwenye TV. Na hata kama ni mwenye hiyo shepu basi kuna kitu cha ziada kichwani. Hili ni gumu kukubalika na ni sababu tulifundishwa kutafuta thamani ya X. Thamani yetu tunafikiri ipo kwenye kufanikiwa kupata thamani ya X. Thamani yetu tunafikiri ipo kwenyei aina ya vitu au watu tulionao.

Kuna watu wanaona kuwa wao ni wa thamani sasa kwa kuwa mume au mke amekuwa WAZIRI. Wanaamini katika thamani ya X. Ulishaona picha ya Michelle Obama na mumewe wakati Obama si "lolote" machoni pa watu? Lakini mwanamke yule alijua ana nini. Akajua kuwa yeye ni FIRST LADY. Alipokuwa akimuona Obama haoni future president anaona MUME WA FIRST LADY MTARAJIWA.
Dada unanielewa?


Sasa wewe mumeo akipewa cheo serikalini unaanza kujitambulisha kama mke wa waziri wa..... Hawa ndo wanawake waliokuwa wanatisha polisi njiani. Eti unajua mi ni nani? Ngoja nimpigie mume wangu sasa. See? Huyu anahisi thamani yake iko katika cheo cha mumewe. Na ndo maana cheo cha mumewe kikikoma anakuwa kama mtu asiye na thamani hata akipita barabarani.

Namheshimu sana dada anaitwa Hoyce Temu. Huyu anajua thamani yake. Amesimama kama yeye. Niliwahi kufanya kazi na kijana anaitwa JACOB MSEKWA yaani huyu jamaa hakuwa na maisha ya kujiweka kama "mtoto wa......". Huyu jamaa alinifundisha kitu kikubwa sana. Alijinasibu kwa utendaji wake wa kazi kiasi kwamba jina la Baba yake halikupewa nafasi kabisa. Alikuwa yeye kama yeye. Lakini ofisi hiyo hiyo kulikuwa na watoto wengine wa "wakubwa" ambao kitu pekee kikubwa kilichowatambulisha ni jina la baba. Walipewa heshima na nidhamu ya woga kwa sababu tu ya nafasi ya mzazi.
So sad.

Pia niliwahi kufanya kazi na dada mmoja anaitwa Madeleine.. huyu ni binti wa  Kimei. Alikuwa akipiga kazi na kujituma pengine kuliko sisi wengine tuliotokea familia "duni". Usingeweza kudhani huyu ni binti wa Kimei kwa hali ya kawaida ya kitanzania. Anajua thamani yake haiko katika jina la  Baba yake. Sitamsahau pia huyu. Lakini wengine unakuta ni mpwa sijui wa mkuu wa kituo cha polisi tu lakini weee mwambie kitu uone.

Na mpaka leo tuna viongozi ambao uongozi wao hauna kitu. Kinachowabeba ni jina alilojenga baba kwa miaka mingi. Basi. Hawakutaka kutafuta thamani yao wao kama wao.
Najua unawajua.

Kutojua thamani zetu ndo kumefanya baadhi yetu kutafuta kwa bidii kuishi Ulaya au Marekani ili tukiongea tusikilizwe. Tusiposikilizwa inatusumbua kweli. Kumbe tunashindwa kujua kuwa thamani yetu haiko kwenye kuishi kwetu Ulaya per se ipo kwenye vitu ambavyo Mungu aliwekeza (invest) ndani yetu. Labda uliwekewa kufundisha kama kina sisi. Labda kuchora kama Masoud Kipanya. Labda kuigiza kama marehemu Kanumba. Au uongozi kama mwalimu Nyerere. Ukiishi thamani yako halisi hata ukifa utasikilizwa. Yani watu wanataka kubadili katiba miaka mingi baada ya kufa kwako lakini bado wanasikiliza kwanza hotuba zako kutafuta ushauri.
Can you imagine?

Usipoishi thamani yako ukafikiri thamani yako ni kuoa mke MKALI au kuolewa na BONGE LA BWANA au ni kupata Masters au kuishi Marekani utashangaa unavyo hivyo lakini bado huthaminiki kivile. Utashangaa Diamond akichepuka inakuwa story hadi BBC wakati wewe hata ufanye nini hakuna anayetaka kujua. Diamond angekuwa mhasibu wa Vodacom leo hii angekuwa na hela nzuri tu lakini hakuna ambaye angetaka kujua sijui kazaa na nani. Sishabikii hayo. No. Nakuonyesha value yako halisi ikikutana na ufahamu sahihi hakika utaongea na nchi itasikia.

So tulitoka huku.....

X + (1⁄2)X + 1 = 100

Tafuta thamani ya X.

Mi nasema sasa huku mtaani acha kutafuta thamani ya X. Tafuta kujua thamani yako. Na kama bado uko shule usiishie tu kutafuta hiyo X ukafurahia umefaulu hesabu. Tafuta thamani yako.

Katika kitu kilichowakwaza ndugu zangu na watu wa karibu ni pale nilipoacha ajira kuanza njia ya ujasiriamali. Nilipoona thamani yangu HALISI haipo kwenye Degree yangu ya sheria au kazi nzuri benki ya kigeni bali nahisi kuna kitu ndani yangu katika kufundisha watu hasa vijana wenzangu. Silipwi chochote lakini furaha ninayopata hapa huwezi kuelewa kirahisi. Najua sasa kuwa nina mchango mkubwa wa mawazo kwa vijana wenzangu kuliko ningekuwa niko zangu mahakamani kuendelea na kazi ya sheria. Sishangai kuwa wapo wasionielewa. Ila tu nawaombea na WAO wagundue thamani zao halisi. Na siyo kutafuta tu thamani zao kupitia X.

Sijui wewe thamani yako iliwekwa kwenye mkono na vidole kama mimi au miguu au mdomo au koo au misuli au kichwani tu huko au kwenye macho. Kuna watu akiona kitu tu anabuni kitu kingine kutokana na alichoona. Kuna mwingine hana macho kama wewe wewe na mimi lakini thamani yake siyo mchezo.

Thamani ya Hellen Keller ilikuwa kwenye kutoona na kutosikia kwake. Akafanikiwa bila macho wala uwezo wa kusikia kuliko mamilioni wenye macho na wenye kusikia vizuri ambao tunataka tu kusikiliza umbea na vitu visivyo na maana.


Niliwahi kusema thamani ya Dan Brown ni kuandika Novel zinazofanya uone maisha upya kabisa na ya Les Brown ni kutoa speech zinazofanya uone maisha upya vile vile. Na wote wamekuwa millionaires.

What about you?

Usifate mkumbo. Yule binti aliyekosa chuo aliniambia kuwa nilimsaidia kutambua kuwa amekuwa kumbe akifata tu mkumbo... na kwamba sasa anahitaji muda wa kukaa na kutafakari juu ya maisha yake.


Point yangu siyo watu wasisome. No. Keller alisoma. Mimi nimesoma nashukuru Mungu.

Point yangu ukasome tena sana tu lakini siyo ili kukamilisha ratiba. Au ili kupata title. Usitafute thamani yako kupitia elimu yako. Thamani yako ni kitu tofauti na elimu ni kitu tofauti.

Thamani yako ni tofauti na mume/mke ni kitu kingine cha kukamilisha hiyo VALUE yako. Sasa usipojua ndo hicho kinachopaswa kukukamilisha tu wewe ndo utakifanya ndo the real thing. Ndo maana unataka a READY-MADE MATERIAL.

Usitafute tu mbinu za kwenda Ulaya hata kama ni kwa kupitia njia za mkato ili na uridhike kuwa na wewe ulishafika Ulaya. Nenda Ulaya ukiwa wewe umeshatambua thamani yako. Hata kama jina lako halijulikani bado but unajitambua. Wanaoenda Ulaya wakiwa wanajitambua hata akirudi anaishi kwa busara siyo labda kujionyesha kama sisi wengine.. Anajua thamani yake haikuwa katika kwenda Ulaya.

Fanya hivi.
Ukiondolewa elimu yako yote, ukanyang'anywa hicho cheo ukaondolewa hizo nyumba na hilo gari utabaki kama NANI?
Hiyo ndo thamani yako.

Ayubu wa kwenye Biblia alijua kuwa THAMANI YAKE HALISI haikuwa kwenye wingi wa mali wala wingi wa wana na mabinti. Thamani yake ilikuwa katika KUMPENDA MUNGU na ndo maana vitu vyote vilipoondoshwa alibaki na simple statement: BWANA ALITOA NA BWANA AMETWAA...... Hata alipougua bado alibaki na thamani yake.


Kifupi alitafuta zaidi thamani yake zaidi kuliko thamani ya X. Na hicho hadi Mungu alijivunia. Mungu hakujivunia wingi wa mali za Ayubu. Lakini sisi tunajivunia wingi wa mali na kuhisi ndo vinatuongezea thamani.

Usijilinganishe na wasio na vitu ukahisi wewe uko juu. Thamani yako iko kwenye CONTRIBUTION  yako kwenye jamii.

Nilipoongea na huyo binti nilimwambia ahakikishe katika maisha yake anakuwa INDISPENSABLE. Yani mtu tegemeo kwenye jamii. Yani watu wakiwa na maswali wanalazimika tu kutafuta majibu kwako watake wasitake. Hapo unakuwa umejenga THAMANI YAKO HALISI. Jamii kukutegemea wewe siyo lazima iwe kwa sababu ya cheo chako au pesa zako. Inawezekana kabisa ukawa huna cheo na watu wakakutegemea. Hapo thamani yako halisi imedhihirika.

Kama cheo  ulichokuwa nacho "kimeEXPIRE" na watu hawakutafuti tena ujue ulipoteza muda kutafuta thamani ya X badala ya kutafuta thamani yako mwenyewe. Hawa ndo ambao ukimuondolea cheo inakuwa ugomvi. Mara mimi nimepigania nchi. Mara mimi hiki. Mara mimi ni muhimu. My friend umuhimu wako huwezi kuitangaza wewe. Wewe ulijisahau ukatafuta thamani ya X ukasahau kutafuta thamani yako. Kuna mawaziri leo hata ukiwashusha vyeo thamani yao kwenye jamii na taifa inajulikana tu. Walijua kutofautisha thamani ya X na thamani yao.

INDISPENSABILITY yako ina maana kuna vitu haviwezi kufanyika bila wewe kushirikishwa kwanza. Siyo kwa sababu ya cheo chako bali by virtue of who you have become. Nakupa mfano wa mwisho. Abraham alikuwa mwenye roho nzuri na ukarimu uliopitiliza kiasi kwamba mpaka alikuwa anaweza kukaribisha wapita njia tu wapate msosi na kupumzika kwake kisha ndo waendelee na safari zao. Yani unakuwa mwema mpaka unaishiwa wa kuwatendea mema unaanza kulazimisha kuwatendea mema wapita njia! Duh. Hii level Mungu mwenyewe akaona hii si mchezo. Huyu mtu siwezi kufanya jambo halafu nimfiche.

Ndo Mungu akamnong'oneza Abrahamu kuhusu mpango wake wa kuiadhibu miji ya Sodoma na Gomora. Tena akaanza kuwaombea watu wa miji hiyo.

See?

Sasa Mungu hakumwambia hizo habari Abrahamu kwa vile Abrahamu alikuwa mtu tajiri. No. Indispensability ya Abrahamu haikuwa kwenye mali bali utu wema wake.

So wewe kama unatafuta mali ili uwe muhimu hapo ni sawa sawa unagongelea msumari kule kwenye ncha.
You're doing it wrong.

Ukitaka kujua angalia watu wanajisikiaje wakisikia majina yafuatayo:


Rugemalila
Bakhressa
Dewji
Rostam


Nani hapa ni INDISPENSABLE?
Yaani ukimtoa huyo lazima umrudishe ili mambo yaende. Na ni nani hata akiondoka watu watamsahau kesho yake tu?

Utakuta watu I'm sure hawatajisikia the same ukiwatajia hayo majina. Kwa nini iwe hivyo wakati hao wote wana pesa?

Issue hapo ni THAMANI ya kila mtu kwenye jamii... Yaani kama ukimnyang'anya pesa zake zote jamii bado itamkubali as a person?
Hiyo ndo thamani yake halisi.

Hapo haijalishi kama ameshatafuta thamani ya X na kuipata. Hapo ni yeye. Thamani yake.

Jichunguze pia.

Are you becoming INDISPENSABLE too au bado unatafuta tu thamani ya X?

Mwisho wa maisha yako utakachowaza sana ni JINA GANI unaacha nyuma. Utaondoka dunia hii ukiacha nini kiishi miaka mingi baada yako? Kwamba ulikuwa na diploma ya ualimu?
Kwani wangapi wanayo?

Ukianza kutafuta thamani yako hutahangaika kujua watu wanakuonaje wala wao wanamiliki nini au wamepiga hatua kiasi gani. Utakuwa more concerned na kujua Mungu aliwekeza nini ndani yako ili uanze kukufanyia kazi mapema ungali na muda bado.

Ajiriwa ndiyo lakini find your real VALUE. Thamani ya Millard Ayo iko wazi. Hakuishia kuajiriwa tu. Alitambua nini Mungu aliweka ndani yake.
Jifunze kwake.

Soma sana tu but find your REAL value.
Tukiondoa elimu yako yote utabaki na nini?

Oa au olewa lakini jua THAMANI yako usije ukaanza kusumbua watu njiani eti, "Unajua mi nani?"

Ukiona mo sijui wewe ni nani ujue hujawa muhimu kwangu. So kaongeze thamani yako nitakujua tu. Au nakosea ndugu zangu? Kwani Max Malipo si unaona mwenyewe thamani yake? Au mpaka akwambie?

That's what I'm talking about.

Achana na thamani ya X saivi hiyo ilikuwa darasani.

Sasa hivi tunabadili swali:


YOU + (1⁄2)YOU + 1 = INDISPENSABILITY

Tafuta thamani ya "YOU".

Ukilipata jibu hapo basi tutakujua sisi wote very soon.


Nakutakia mema!

#FourteenSix

Till next time.


Semper Fi,

Andrea G. Muhozya
Dar es Salaam, Tanzania
East Africa
WhatsApp +255 788 366 511
www.andreamuhozya.blogspot.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni