Jumatatu, 17 Julai 2017

HAKUNA MTU ASIYEWEZA KUFANIKIWA KIUCHUMI #AKIAMUA

HAKUNA MTU ASIYEWEZA KUFANIKIWA KIUCHUMI AKIAMUA


Siku kadhaa zilizopita nilikutana na hawa kina dada wawili mtaani (mitaa ya Sinza) wakiwa wamepumzika baada ya kazi kubwa ya kutembeza mboga za majani mtaani.


Walikuwa wamechoka hakika na walikuwa wamekaa mahali dukani wakiwa wameagiza zao soda baridi kushushia kidogo na labda kulainisha koo kwa sababu ya kazi nzito ya kutembea juani na huku ukiita kwa sauti: "Haya jamani mchicha, mnafu, matembele, mchichaaaaa".

Niliwasalimia na kukatisha safari yangu   ili nikae nao pia ili niendelee kujifunza maisha ningali hapa duniani.

Ama baada ya salamu na maneno mawili matatu ya "Breaking the Ice" nikaanza kureason nao mambo ya biashara na hasa biashara yao.

Mimi:
Hebu niambieni nyinyi changamoto yenu hasa ni nini kwenye hii biashara?

Mmoja wao:
Dah kakangu changamoto ni nyingi mno lakini kubwa ni kwamba watu siku hizi wanaogopa kula mboga za majani si unasikia sijui serikali wanasema mboga zisilimwe sehemu za maji yenye sumu?

Mimi:
Oh poleni nimesikia sikia hivyo pia hasa kuhusu bonde la Msimbazi na Mlalakuwa. Kwani nyie mboga zenu mnatoa huko pia?

Wao:
Hapana sisi tunatoa huko Tegeta! Lakini bado wateja hawaamini wanaogopa tu kwa hiyo kwa kweli ni changamoto.

Mimi:
Sasa kama hali ndo hiyo mnajiandaaje mbeleni mfano serikali ikisema mboga mboga zisiuzwe mtaani ili kuepusha labda magonjwa ya mlipuko nyie mtafanya nini kwa kipindi hicho cha marufuku ya aina hiyo.

Wao:
Eeh kakangu sisi tunaomba tu yasifike huko maana humu ndo tunajipatia kipato chetu na kusaidia mambo ya familia yanaenda. Kwa hiyo serikali isifike huko watusaidie kwa hilo.

(Nikaona nibadili uelekeo wa maswali kidogo...)

Mimi:
Aisee. Kumbe biashara siyo mbaya ee. Safi sana. Kwani kwa mfano kwa kawaida kwa siku mnaweza kutengeneza faida ya shilingi ngapi?

Wao:
Kama siku ikiwa ngumu faida sh 25,000 hivi lakini ikiwa nzuri ni sh 45,000/- mpaka 50,000/- kwa siku!

(Hapo nikawaza upya kabisa. Maana average ya tuseme 35,000/- tu kwa siku 6 wanazofanya kazi ni sh 210,000 kwa wiki. Kwa mwezi ni kama Tshs 840,000/-. Usiwachukulie poa kivile ujue..)

So, Mimi:
Aisee, hongereni sana. Nimeipenda sana bidii yenu. Kumbe mambo siyo mabaya sana. Sasa mna mpango gani na kipato kikubwa sana namna hiyo ambacho mnaingiza kwa sasa? Mnasomesha?

Wao:
Tunashukuru serikali kwa shule za msingi sasa ni bure lakini tuna wa sekondari ndo humu humu tunapata kaka. Tunashukuru Mungu.
(Mmoja wao) mfano mimi mwanangu (akataja jina) anasoma tuition moja na watoto ambao wazazi wao wanafanya kazi kwenye mabenki na hata serikalini.  Kwa kweli Tunashukuru.  Ila ndo hela inaishia huko na matumizi mengine.

Mimi:
Hongera sana. Mnafanya mambo makubwa sana nyie hivi watoto wenu wanajua kwamba nyinyi mnatenda maajabu makubwa namna hii?

Wao:
(Wakacheka kidogo)
Ndiyo wanajua. (Mmoja wao) Wanajua tunavyohangaika mfano mimi mwanangu wa sekondari alirudi nyumbani juzi akaniuliza "Mama nasikia serikali inasema mboga mboga zina sumu, sasa mama wakiwakataza kuuza mi ntapata ada kweli?"

(Alikuwa emotional sana wakati akiongea hivyo so nikaona nikienda huko inaweza kumfanya hata alienda machozi.. si lengo langu for any reason)

Mimi:
Aisee. Sasa mnatamani watoto wenu waje wafanye kazi hii mnayoifanya nyinyi huko mbeleni?

Wao:
Eeh hata! Hii kazi ngumu tunawaambia watie bidii shuleni tu ili wasije wakafanya kazi hii. Migongo inatuuma tukirudi nyumbani, miguu, huku watu mara walalamike mboga zina sumu.

Mimi:
Mna muda gani na hii kazi?

Wao:
Miaka mingi kwa kweli. Zaidi ya tisa.

Mimi:
Wow! Sasa kama hamtaki watoto wenu waje wafanye hiki mnachofanya mmewaandalia akiba yoyote kifedha?

Wao:
Eeh kaka hivi hiyo akiba inatoka wapi hela yenyewe haitoshi ndugu yangu.

Mimi:
Mmesema mnaweza kupata mpaka elfu 45 nk. Sasa hivi unajua ukiweka tu akiba ya sh 5,000/- kila siku unajua kwa siku 10 itakuwa sh 50,000/-? Hiyo ni elfu 50 ambayo ipo tu. Na kwa siku 100 unajua ni sh 500,000/? Na unajua siku 100 ni sawa na miezi mitatu tu na siku 10?

(Nikaona kama "network inasearch kidogo". Nikaendelea kidogo)...

Mimi:
Hivi unajisikiaje dadangu ukiwa na ndugu yako kila baada ya miezi mitatu na siku 10 anakutumia laki 5? Unaweza kufanya mambo mangapi na laki 5?
Lakini mtegemea cha ndugu huwa anafanyaje dada zangu?

Wao:
Anakufa masikini kakangu.. (Kwa huzuni kidogo)

Mimi:
Sasa unaonaje ukajipa mwenyewe hiyo laki 5 kwa kutunza elfu 5 tu kwa siku hiyo elfu 5 ambayo haiathiri sana maisha yako kivile maana unabaki na kati ya elfu 20 hadi 40 kwa siku kwa sababu nyinyi mna uwezo wa kipato cha kila siku. Kati yenu yupo ambaye hawezi kuweka pembeni sh elfu 5?

Wao:
Kwa kweli hakuna..

Mimi:
Sasa TUSAHAU miaka tisa au hata miwili iliyopita. Tuangalie miwili au tisa ijayo. Kwa haraka haraka mwaka ukiisha utakuwa umeweka sh 1,500,000/- ya elfu tano tu ile nyingine unaendelea kutumia.
Baada ya miaka mitano tu una milioni 7,500,000. Fikiria miaka mitano iliyopita hadi sasa kuna milioni 7 na nusu ambayo hukuitunza kutoka kipato chako cha kila siku imepotea.

Mimi:
Ukipata milioni 7 na nusu ukaanza kuwakopesha wauzaji mboga wenzako unajua utakuza kipato chako mara dufu. Kuna Microfinance zilikuwa zinakopesha tu pesa lakini mpaka zimegeuka kuwa benki rasmi sasa (nikawatajia moja). Kumbe hata nyinyi mnaweza na biashara ya mboga unapumzika kabisa miaka mitano tu ijayo. Na mtoto aliyekuwa kidato cha pili hapo atakosa ada ya Chuo? Hata akipata mkopo nusu au robo tu utashindwa kumsaidia mahitaji mengine hapo juu?
Japo ni vizuri umsomeshe tu kwa pesa yako hiyo ya kuweka. Hivi unajua mzazi anayeshangilia mtoto wake kupata mkopo kwa upande mwingine anashangilia mtoto wake kuhitimu akiwa na deni kabla hata hajaanza kuingiza kipato? Watoto wa matajiri wanahitimu bila madeni.  Wa maskini wanahitimu na madeni. Hiyo ndo tofauti mojawapo. Wanaanza maisha wakiwa level tofauti za kiuchumi. Ni vigumu waje kulingana baadaye.

Wao:
Dah kaka yani umetufanya tuone tumepoteza pesa hata kunywa hizi soda jamani. Yani tungeyajua haya zamani mbona tungekuwa mbali mno! Jamani bora hata ulipita na ukatusalimia tumejifunza mengi mno.

Mimi:
Usijali. Hatua zetu tukinuia mema huongozwa na Mungu. So tumshukuru Mungu tu dada zangu.


Wao:
Sasa tunaanzaje?

Mimi:
Kuna wataalamu wa mambo ya uwekaji akiba.  Watu wa mabenki nk. Mkiwakosa niambieni nitawatafutia. Wao wanajua nini ufanye na hiyo sh 5,000 uiweke tu na huwezi kuitoa hadi muda mliokubaliana utimie. Cha msingi siyo hiyo elfu 5 bali ni #NIDHAMU. Hiyo nidhamu watoto wako wakiijifunza wakaibeba na elimu watakayokuwa nayo familia yako na kizazi chako baada yako hawataamini kuwa kuna muuza mboga mboga mitaani ndo chanzo cha wao kufanikiwa.

Cha msingi usijiangalie wewe. Focus kwenye kizazi chako baada yako. Fikiria hali itakuwaje ukiwa mzee na unaona watoto wako na wajukuu zako wamebeba nidhamu nzuri kabisa ya fedha ambayo uliianzisha wewe kwa kuuza mboga mboga na kuweka sh 5,000 tu kwa siku.
Fikiria utakavyokumbuka elfu 5 yako ya kwanza, fikiria inavyoonekana ndogo lakini ilivyobeba utajiri wa vizazi na vizazi.

Wao:
Dah aisee kaka asante Mungu akubariki sana. Yani tunaomba tuje tukae tena tumependa sana mafunzo yako.

Mimi:
Asanteni sana dada zangu aisee.

Mwenye duka (Mangi):
Aisee huwa unatoa semina wapi jamaangu? Maana naona una mambo mazu..! Mazuri aisee.

Mimi:
Nitakuja tuongee zaidi ngoja nawahi mahali maana hata hivyo nilitaka kuwasalimia tu hawa dada zangu.

Kina dada:
Basi tupige hata picha ya ukumbusho maana leo tumepata elimu nzuri sana.(Mangi akawa mpigapicha kwa muda)

Nikawaaga na kuendelea na safari yangu.


Nitawatafuta tena hawa dada zangu nijue wanaendeleaje.....

Usidharau kipato chako....!#ThreeSixteen

Semper Fi,

Andrea G. Muhozya
Dar es Salaam, Tanzania,
East Africa
#WhatsApp +255 788 366 511
Blog: www.andreamuhozya.blogspot.com***The End.****

Maoni 1 :

 1. Je! Unahitaji mkopo wa haraka, mrefu au mrefu kwa kiwango cha riba cha chini
  chini ya 3%?

  Gregowenloanfirm1@gmail.com

  Tunatoa mkopo wa biashara:
  Mkopo wa kibinafsi:
  Mkopo wa nyumbani:
  Mkopo wa Auto:
  Mkopo wa mwanafunzi:
  Mkopo wa kuimarisha madeni: e.t.c.

  Haijalishi score.we yako ya mikopo ni uhakika katika kutoa nje
  huduma za kifedha kwa wateja wetu wengi duniani kote.
  Kwa vifurushi vyenye mikopo rahisi,
  Mikopo inaweza kusindika na kuhamishiwa kwa akopaye ndani
  muda mfupi iwezekanavyo.
   
  Ikiwa unahitaji kuwasiliana na mkopo haraka kupitia barua pepe:

  gregowenloanfirm1@gmail.com

  3% ya kuaminika mkopo kutoa uhakika.

  JibuFuta